Thursday, June 10, 2010

HISTORIA YA KOMBE LA DUNIA

HISTORIA ya kombe iliandikwa kwa mara ya kwanza mwaka 1928 wakati Rais wa FIFA wakati huo, Jules Rimet alipoamua kuandaa michuano mikubwa zaidi duniani inayohusisha mataifa mbalimbali.

Ufunguzi wa michuano hiyo ilifanyika miaka miwili baadaye mnamo mwaka 1930 nchini Uruguay na timu 13 zilialikwa kushiriki michuano hiyo.Kuanzia hapo, FIFA ilifanikiwa kubadilisha miundo mbalimbali ya michuano katika miaka ya nyuma.

Timu 32 zinapatikana baada ya mchakato wa mechi za kufuzu ambazo zinashirikisha timu kutoka mataifa 200 duniani kote.Kabla ya kombe la dunia Mechi ya kwanza ya kimataifa ya soka duniani ilichezwa mwaka 1872 kati ya England dhidi ya Scotland ingawa katika kipindi hicho ilikuwa ni mara chache kwa mchezo wa soka kuchezwa nje ya Uingereza.

Hata hivyo, kuanzia mwaka 1900 mchezo wa soka ulipata umaarufu duniani kote na vyama vingi vya soka vikaanzishwa. Mechi ya kwanza rasmi ya kimataifa kuchezwa nje ya Uingereza ilikuwa kati ya Ufaransa na Ubelgiji ambayo ilichezwa Paris,Mei 1904.

Mchezo huo ulisababisha kuanzishwa kwa Shirikisho la soka duniani (FIFA) Mei 22, 1904. FIFA ilianzishwa na Vyama vya soka vya Ufaransa, Ubelgiji, Denmark,Uholanzi, Hispania, Sweden na Uswisi huku Ujerumani ikiomba kujiunga.


Huku mchezo wa soka ukianza kupata umaarufu, mchezo huu ulianza kutambulika kama mchezo rasmi wa michezo ya Olimpiki mwaka 1904 katika kipindi cha majira ya joto.Baadaye FIFA ilikuja kusimamiamichuano ya Olimpiki katika upande wa soka mnamo kipindi cha majira ya joto mwaka 1908.

Wakati huo mchezo wa soka ulikuwa unajumuisha wachezaji wa ridhaa tupu na ulikuwa unachukuliwa kama mchezo wa maonesho tu kuliko ushindani.

Timu ya taifa ya soka ya ridhaa ya England ilishinda michuano hiyo ya Olimpiki mwaka 1908 pamoja na ile ya mwaka 1912.Baadaye FIFA ilijaribu kuanzisha michuano mingine ya soka ya kimataifa bila ya kuhusisha michuano ya Olimpiki.

Majaribio haya yalianzishwa mwaka 1906 nchini Uswisi.Hizi zilikuwa siku za mwanzo za soka la kimataifa na historia rasmi ya FIFA inaelezea kwamba mkutano huo ulishindwa kuzaa matunda.

Huku michuano ya Olimpiki ikiendelea kushindanisha timu za ridhaa, michuano ya timu za kulipwa nayo ikaanza.Michuano ya Torneo Internazionale Stampa Sportiva, ilifanyika jijini Turin, Italia mwaka 1908. Hii ilikuwa ya kwanza kabisa na mwaka uliofuata Sir Thomas Lipton alianzisha michuano iliyofahamika kama ‘Kombe la Sir Thomas Lipton’ iliyofanyika Turin.

Michuano hiyo ilikuwa inashirikisha klabu na si timu za taifa. Klabu moja ilikuwa inawakilisha taifa zima nyumbani. Kwa sababu hii, hakuna michuano ambayo ilichukuliwa kama mfano wa kombe la dunia kabla yauwepo wa kombe la dunia.

Mwaka 1914, FIFA ilikubali kuitambua michuano ya Olimpiki kama ‘Michuano ya dunia ya ridhaa’ na ilikubali kuwajibika kuandaa michuano hiyo.Hii ilisababisha iwepo michuano ya kwanza ya kimataifa ya soka katika Olimpiki ya mwaka 1920 ambapo Ubelgiji alichukua.Uruguay ikashinda michuano yaOlimpiki ya mwaka 1924 na 1928.

Mnamo mwaka 1928 FIFA ilichukua uamuzi wa kuandaa michuano yao wenyewe.Huku Uruguay ikiwa imeshinda mara mbili michuano ya Olimpiki na ikijiandaa kusheherekea mwaka mmoja baada ya kupata uhuru, FIFA iliamua kuipa Uruguay uenyeji wa michuano hiyo ya kwanza ya kombe la dunia 1930.Michuano ya kwanza ya kombe la dunia

Michuano ya mwaka 1932 ya kipindi cha majira ya joto ilifanyika jijini Los Angeles na haikupanga kuujumuisha mchezo wa soka kutokana na umaarufu mdogo wa mchezo wa soka Marekani.

FIFA na IOC zilikuwa zimeshindwa kukubaliana masuala fulani ya michuano hiyo, kwa hiyo mchezo wa soka ukaondolewa katika orodha ya michezo ya mwaka huo.

Rais wa FIFA, Jules Rimet ndiye akaamua kuandaa michuano hiyo iliyofanyika Uruguay mwaka 1930.Vyama kadhaa vya soka viliteuliwa kupeleka timu zao na huku chaguo la uenyeji likienda kwa Uruguay. Hiyo ilimaanisha kuwa timu nyingi za Ulaya zingelazimika kukatiza Bahari ya Atlantic kucheza michuano hiyo.

Hakuna timu yoyote ya Ulaya ambayo ilithibitisha kupeleka timu mpaka ilipobaki miezi miwili kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.Kwa juhudi binafsi za Rimet alifanikiwa kuzishawishi nchi za Ubelgiji, Ufaransa, Romania na Yugoslavia kusafiri.

Kwa ujumla nchi 13 zilishiriki michuano hiyo huku saba zikitoka Amerika Kusini,nne kutoka Ulaya na mbili kutoka Amerika Kaskazini.

Mechi mbili za kwanza zilichezwa mfululizo huku Ufaransa ikiichapa Mexico 4-1 na Marekani ikiichapa Ubelgiji 3-0.Bao la kwanza katika historia ya kombe la dunia lilifungwa na Lucien Laurent wa Ufaransa.

Siku nne baadaye dunia ilishuhudia Bert Patenaude akifunga mabao matatu kwa mpigo (Hat trick) katika ushindi wa 3-0 wa Marekani dhidi ya Paraguay.Katika pambano la fainali lililochezwa Montevideo, wenyeji Uruguay waliichapa Argentina 4-2 mbele ya mashabiki 93,000 na kuingia katika historia ya timu iliyotwaa kwa mara ya kwanza taji holo.


Hivyo ndivyo michuano ya kombe la dunia ilivyoanza.





Madiba akifurahia kombe la dunia. Hongera!!!!!

Je wajua haya kuhusu kombe la Dunia?


-Michuano ya kombe la dunia imechezwa mara 17 lakini mpaka sasa ni nchi sita tu zilizowahi kutwaa kombe hilo.

-Mechi ambayo ilihudhuriwa na mashabiki kidogo zaidi katika kombe la dunia ni kati ya Romania na Peru katika fainali za mwaka 1930 nchini Uruguay. Waliingia mashabiki 300 tu.

-Hakuna nchi yoyote ya Ulaya iliyowahi kutwaa kombe la dunia nje ya bara la Ulaya.

-Diego Maradona ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi akiwa na kitambaa cha unahodha. Alicheza mechi 16 kama nahodha.

-Fainali za kombe la dunia mwaka 2002 ziliandaliwa katika nchi za Japan na Korea Kusini. Ugomvi mkubwa baina yao ulikuwa ni jina la nchi gani litokee kwanza katika tiketi za mechi hizo.

-Hakuna nchi yoyote ambayo iliwahi kufungwa pambano lake la kwanza na kutwaa kombe la dunia.

-Julai 31 imetajwa kama siku ya mapumziko nchini Uruguay baada ya taifa hilo kutwaa kombe la dunia lilipofanyika mara ya kwanza.

-Tabia ya wachezaji kubadilishana jezi uwanjani ilipigwa marufuku mwaka 1986 na FIFA kwa sababu haikupenda kuwaona wachezaji wakitoka nje ya uwanja vifua wazi.

-Matokeo mengi katika kombe la dunia ni yale ya 1-0
Rigobert Song wa Cameroon ndiye mchezaji aliyepewa kadi nyekundu katika michuano miwili ya kombe la dunia mfulilizo. Alipewa dhidi ya Brazil mwaka 1994 na akapewa dhidi yaChile mwaka 1998.

-Mchezaji aliyefunga mabao mengi ya kichwa katika fainali za kombe la dunia ni Miloslav Klose wa Ujerumani.Katika fainali za mwaka 2002 alifunga mabao matano kwa kichwa.

-Pambano la kombe la dunia mwaka 1970 kati El Savador na Honduras lilikuwa na upinzani mkubwa kiasi kwamba nchi hizo ziliingia katika vita ya mtutu kwa siku tatu.

-Ni mabara mawili tu ambayo yamewahi kushinda kombe la dunia,hayo ni Ulaya na Amerika Kusini.Ulaya imeshinda mara nane na Amerika Kusini imeshinda tisa.Mabara ya Asia, Afrika, Amerika Kaskazini na Kati yote yameshindwa kutwaa taji hili.

-Brazil ni nchi pekee iliyocheza michuano yote ya fainali za kombe dunia.

-Brazil ndiyo nchi pekee iliyofunga idadi kubwa ya mabao katika fainali za kombe la dunia. Imefunga mabao 173.

NCHI ZILIZOTWAA KOMBE LA DUNIA 1930 HADI 2006


1930 Ilifanyika Uruguay, fainali ni kati ya Uruguay vs Argentina 4-2

1934 Ilifanyika Italia, fainali ni kati ya Italia vs Czechoslovakia 2-1

1938 Ilifanyika Ufaransa, fainali ni kati ya Italia vs Hungary 4-2

1950 Ilifanyika Brazil, fainali ni kati ya Uruguay vs Brazil 2-1

1954 Ilifayika Uswisi, fainali ni kati ya Ujerumani vs Hungary 3-2

1958 Ilifanyika Sweden, fainali ni kati ya Brazil vs Sweden 5-2

1962 Ilifanyika Chile, fainali ni kati ya Brazil vs Czechoslovakia 3-1

1966 Ilifanyika England, fainali ni kati ya England vs Ujerumani 4-2 (pen)

1970 Ilifanyika Mexico, fainali ni kati ya Brazil vs Italia 4-1

1974 Ilifanyika Ujerumani, fainali ni kati ya Uholanzi vs Ujerumani 1-2

1978 Ilifanyika Argentina, fainali ni kati ya Argentina vs Uholanzi 3-1 (pen)

1982 Ilifanyika Hispania, fainali ni kati ya Italia vs Ujerumani 3-1

1986 Ilifanyika Mexico, fainalili ni kati ya Argentina vs Ujerumani 3-2

1990 Ilifanyika Italia, fainali ni kati ya Ujerumani vs Argentina 1-0

1994 Ilifanyika Marekani, fainali ni kati ya Brazil vs Italia 3-2 (pen)

1998 Ilifanyika Ufaransa, fainali ni kati ya Brazil vs Ufaransa 0-3

2002 Ilifanyika Korea/Japan, fainali ni kati ya Ujerumani vs Brazil 0-2

2006 Ilifanyika ujerumani, fainali ni kati ya Italia vs Ufaransa 5-3 (pen)

Fainali hizi ni mara ya kwanza kuchezwa katika bara la afrika ingawa zipo baadhi ya timu za taifa kutoka afrika zikishiriki. Michuano hii itafunguliwa na raisi wa kwanza wa Afrika kusini na kushuhudiwa na viongozi wakubwa duniani kama Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Kin Moon. Makundi ambayo yanategemewa kukipiga tarehe kumi na moja mwezi huu kule Afrika kusini ni kama ifuatavyo;


Kundi A. Afrika Kusini, Mexico, Uruguay na Ufaransa.
Kundi B. Argentina, Nigeria, Korea Kusini na Ugiriki.
Kundi C. England, Marekani, Algeria na Slovenia.
Kundi D. Ujerumani, Australia, Serbia na Ghana.
Kundi E. Uholanzi, Denmark, Japan na Cameroon.
Kundi F. Italia, Paraguay, New Zealand na Slovakia.
Kundi G. Brazil, Korea Kaskazini, Ivory Coast na Ureno.
Kundi H. Hispania, Uswisi, Honduras na Chile.


Viwanja vya Afrika kusini vitakavyokuwa na shughuli.

Cheki vikosi vitakavyoumana kuanzia tarehe 11.06.2010










Ni hayo tu kwa leo kwa lengo la kukumbusha wapi tumetokea na wapi tunaelekea na nini vinatokea katika mchakato wote wa kombe la dunia.
Tucheki kwa raha zetu....................................................................................................!!!!!!



No comments:

Post a Comment