Friday, June 11, 2010

MECHI ZA MWANZO FAINALI YA KOMBE LA DUNIA KUSHINDWA KUONESHANA UBABE

Mechi za ufunguzi wa fainali za kombe la dunia zilizoanza hapo jana, zimeshindwa kuoneshana ubabe baada ya kutoka sare.

Wenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia, Afrika Kusini, wameanza michuano hiyo kwa matumaini baada ya kutoka sare ya 1-1 na Mexico ingawa timu ya Mexico wenye uzoefu mkubwa wa kucheza katika Kombe la Dunia walianza kwa kumiliki mpira kwa kipindi kirefu, lakini walishindwa kumalizia nafasi zilizopatikana.

Baada ya mapumziko, kocha wa Afrika Kusini, Carlos Alberto Parreira, alifanya mabadiliko kwa kumtoa Lucas Thwala na kumwingiza Tsepo Masilela,mabadiliko yalizaa matunda wakati Siphiwe Tshabalala, kiungo wa Kaizer Chiefs, alipotikisa nyavu katika dakika ya 55 kuipatia Afrika Kusini goli la kuongoza.


Mchezaji wa Afrika kusini Siphiwe Tshabalala alipopiga shuti kali nakuipatia Afrika kusini goli la kwanza.

Goli hilo lilishangiliwa kwa mbwembwe zote zilizoambatana na dansi kavu kavu wakati wachezaji walipokusanyika pembeni.

Bahati mbaya kwa Afrika Kusini, kosa la kushindwa kuwakaba wachezaji wa Mexico katika eneo la hatari lilitoa fursa kwa Rafael Marques kusawazisha katika dakika ya 79.

Wakati hoho huo,Ufaransa na Uruguay zimetoka sare 0-0 kwenye mechi ya pili ya kundi A.

Uruguay walimaliza mchuano wakiwa wachezaji 10 baada ya Nicholas Lodeiro kupewa kadi nyekundu alipomchezea vibaya mlinzi wa Ufaransa, Bacary Sagna.

Ufaransa walifanya mashambulizi mengi bila mafanikio, na katika kipindi cha pili walifanya mabadiliko, akaingia nahodha wao Thierry Henry badala ya Nicholas Anelka, lakini lango la Uruguay likawa halifunguki.

Mkwaju mkali wa mshambuliaji wa Atletico Madrid, Diego Forlan, uliokolewa na kipa wa Ufaransa katika kipindi cha kwanza.


Hii ni moja kati ya mashambulizi kati ya timu ya ufaransa na Uruguay.

Michuano hiyo ya kombe la dunia inaingia katika siku ya pili ya kundi B, wakati leo Nigeria wanachuana na Argentina katika uwanja wa Ellis Park mjini Johanesburg ikifuatiwa na mechi kati ya Korea Kusini na Ugiriki.

Kocha wa Argentina, Diego Maradona, amesema anakusudia kuchezesha washambuliaji watatu dhidi ya Nigeria, na anatarajiwa kuwapanga mchezaji bora duniani, Lionel Messi wa Barcelona, Carlos Tevez wa Manchester City na mshambuliaji wa Real Madrid, Gonzalo Higuai.

Nigeria itawategemea washambuliaji wao wanaocheza Ulaya; nahodha Kanu Nwankwo anayeichezea Portsmouth, Yakubu Ayegbeni wa Everton, Obafemi Martins wa klabu ya Wolfsburg pamoja na Peter Osaze na Chinedu Obasi. Hii ni mara ya tatu kwa Kanu kushiriki Kombe la Dunia.

Tukutane baadaye katika ile pembe nne.......................................................




No comments:

Post a Comment